Watu wasiopungua 14 wameuawa katika shambulio la wapiganaji katika kambi ya wakimbizi wa ndani mkoa wa Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, vyombo vya habari vya maeneo hayo vilisema.
Shambulio hilo katika eneo la Djugu limetokea nyakati za asubuhi wakati wakimbizi hao wa ndani wakielekea kwenye mashamba yaliyoko vijiji vya karibu, kulingana na taarifa.
Redio ya Umoja wa Mataifa, iliyozungumza na walioshuhudia, wanasema waliouawa walikuwa wakulima na walidai kuwa mashambulizi hayo yametekelezwa na kundi la wapiganaji la CODECO.
“Walioshuhudia wanasema kuwa wapiganaji hao waliwavamia, kuwafyatulia risasi na kuwachoma kwa visu. Idadi kamili ya waliouawa bado haijafahamika kutokana na ugumu wa kufikia sehemu hiyo,” taarifa hiyo ilisema.
Hakukuwa na mawasiliano rasmi kuhusu tukio hilo.
Lakini kufuatia mashambulizi hayo, kumekuwa na hofu katika kambi ya Rhoo, ambayo ina maelfu ya wakimbizi wa ndani, taarifa hiyo ilisema.
Viongozi wa mashirika yasiyokuwa ya serikali ya maeneo hayo wanasema jeshi linahitaji kuingilia kati kwa haraka kuhakikisha usalama katika eneo hilo.
Kumekuwa na mapigano mabaya nchini DRC kwa muda mrefu na kusababisha hali mbaya sana kwa watu, huku watu milioni 7 wakiwa wameondolewa kwenye makazi yao nchini humo,kulingana na Umoja wa Mataifa.
Makundi ya wapiganaji yamekuwa yakishambulia raia kote mashariki mwa Congo. Mwezi Julai Umoja wa Mataifa ulitoa taarifa ya mashambulizi ya mauaji yaliyofanywa na waasi wa ADF, CODECO na wapiganaji wa Raia Mutomboki/Wazalendo huko Ituri, Kivu Kusini na Kivu Kaskazini.