Watu milioni mbili wanaoishi Goma wako chini ya kivuli cha Mlima Nyiragongo, moja ya volkano zilizo hai duniani.
Kwa wengi, sura ya mlima huu mrefu unaotanda juu ya mji huu wenye shughuli nyingi katika jimbo la Kivu Kaskazini ni mchanganyiko wa uzuri na hofu.
Josué Aruna mara nyingi hupata faraja katika misitu ya Hifadhi ya Taifa ya Virunga, akivutiwa na umbo la kivuli cha mlima wa volkano. Mara kwa mara, mawazo yake hurudi usiku wa Mei 22, 2021, wakati Nyiragongo ilipoachilia ghadhabu yake kwa Goma.
Saa 12 jioni kwa saa za eneo hilo, lava iliyochemka ilitoka tumboni mwa mlima na kutiririka kwa kasi ya karibu kilomita 100 kwa saa. Anga liligeuka kuwa rangi nyekundu kama damu.
"Hatukuwa mbali na Nyiragongo," Aruna anakumbuka alipokuwa akizungumza na TRT Afrika. "Ilikuwa giza, na tuliona lava – kama mafuriko ya moto – yakitiririka chini ya mlima."
Familia zilitoroka kwa miguu, zikibeba magodoro na vyombo vya kupikia huku mto wa miamba iliyoyeyuka ukielekea mjini, ukichoma vijiji njiani.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi (UNHCR) liliripoti kuwa zaidi ya wakazi 400,000 wa Goma walilazimika kukimbia makazi yao.
Aruna, ambaye hapo awali alishuhudia nguvu za uharibifu za Nyiragongo mwaka 2002, alikuwa amejiandaa kwa tukio hili kwa miaka 19.
"Familia yangu ilipata pigo kubwa wakati wa mlipuko wa 2002," anaambia TRT Afrika. "Tulipoteza kila kitu. Wengi wa jamaa zangu waliishi katika kambi za wakimbizi wa ndani, ambapo hali ya maisha ilikuwa mbaya."
Msaada wa jamii
Mwaka 2016, Aruna alianzisha Shirika la Uhifadhi wa Bonde la Kongo (CBCS), shirika la kiraia linalolenga kusaidia raia kujiandaa na kuishi wakati wa majanga ya asili.
"Sisi ni shirika la kijamii, tunawafundisha watu jinsi ya kujiandaa, na kuunda njia za kuhamishwa zilizotambuliwa mapema zenye alama na matengenezo ya mara kwa mara. Tunaanzisha maeneo salama katika shule, makanisa na vituo vilivyojengwa maalum mbali na maeneo hatarishi. Pia tunatoa msaada wa usafiri, hasa kwa makundi yaliyo hatarini (watoto, wazee, na walemavu)," anaeleza Aruna, ambaye ni mkurugenzi wa shirika hilo nchini.
Nyiragongo imepasuka angalau mara 34 tangu mwaka 1882. Mlipuko wa 2002 ulikuwa mbaya zaidi, ukisababisha vifo vya watu wasiopungua 250.
Aruna anasema masomo yaliyopatikana kutokana na janga hilo yalisaidia shirika lake kuunda mpango wa kukabiliana na milipuko ya baadaye.
"Tulishirikiana na huduma za dharura za serikali ya DRC kusaidia kuwaandaa wakazi wa Goma kwa hali yoyote. Kwa hivyo, mlipuko ulipotokea tena, watu walijua cha kufanya. Walihama haraka," anasema Aruna kwa TRT Afrika. "Ninaamini hili liliokoa maisha ya wengi."
CBCS pia ilitoa msaada wa kifedha kwa familia ambazo bado zilikuwa zikisubiri msaada rasmi, ikiwa ni pamoja na kaya zenye mama wajawazito au wanaonyonyesha peke yao na familia zenye kipato cha chini zinazopata chini ya dola 10 za Marekani kwa mwezi.
Shirika hilo lilitoa chakula na dola 20 kwa kila mnufaika ili kugharamia mahitaji ya msingi.
"Tuliweza kukusanya fedha kutoka kwa biashara ndogo ndogo tulizoendesha ndani ya shirika, ikiwa ni pamoja na benki ya mbegu na huduma nyingine zinazohusiana na kilimo. Msaada wa kifedha ulikuwa mdogo, lakini ulikuwa na maana kubwa kwa watu waliopoteza kila kitu," anasema Aruna.
Msumeno unaokata pande mbili
Mlipuko wa 2021 ulitokea wakati ambapo maisha ya wengi katika eneo hilo tayari yalikuwa yamevurugwa na migogoro. Zaidi ya watu milioni mbili walikuwa wamekimbia makazi yao kutokana na vurugu zilizofanywa na makundi ya waasi, hasa M23, katika jimbo la Kivu Kaskazini.
Watu wengi wameanza kurejea taratibu, lakini maisha Goma bado hayana uhakika.
"Tunakabiliwa kila mara na vitisho viwili vya mauti," anasema Aruna. "Migogoro ya silaha upande mmoja na moja ya volkano zinazofanya kazi zaidi duniani upande mwingine. Kila siku, tunamwomba Mungu atulinde."
Kwa kuwa Kituo cha Uangalizi wa Volkano cha Goma, ambacho kimepewa jukumu la kufuatilia mitetemeko na kutoa tahadhari, kimeathiriwa na ukosefu wa fedha kwa miaka mingi na migogoro inayoendelea, mifumo ya tahadhari ya mapema haifanyi kazi au haipo kabisa.
"Sasa, tunategemea zaidi hisia. Kile kidogo tunachoweza kufanya kama shirika ni kusaidia watu wengi iwezekanavyo kujiandaa kwa mlipuko ujao," Aruna anasema kwa TRT Afrika.